POLISI WACHUNGUZA KIFO CHA MWANABLOGU WA LINDA MWANANCHI
Polisi wanachunguza kifo cha Susan Ndieyira, mwenye umri wa miaka 33, aliyefariki baada ya kuanguka kutoka juu ya jengo la makazi eneo la Tassia, Embakasi, jijini Nairobi.
Mwanablogu huyo wa kisiasa kutoka Bungoma, aliyekuwa akiunga mkono vuguvugu la Linda Mwananchi, alipata majeraha makubwa kichwani na kufariki akiwa njiani kupelekwa hospitalini.
Familia yake inasema alikuwa amepanda juu ya jengo kutundika nguo zilizofuliwa, baada ya kulalamikia maumivu ya kifua na kizunguzungu. Hata hivyo, madai ya mitandaoni kuwa huenda alisukumwa yameibua maswali kuhusu mazingira ya kifo chake.
Imetayarishwa na Cyrus Sifuna

