KAGWE AKOSOA ONGEZEKO LA USHURU DUNIANI, AITAKA AFRIKA KUDHIBITI MAUZO YA NJE YA MAZAO
Waziri wa Kilimo chini Mutahi Kagwe ametoa wito kwa mataifa ya Afrika kukabiliana na kile anachokitaja kuwa kitendo kisicho cha haki duniani cha kupandisha ushuru, ambapo masoko yaliyoendelea huagiza bidhaa ghafi za kilimo kwa ushuru wa chini au sifuri lakini hutoza ushuru wa juu kwa bidhaa sawa pindi zinapochakatwa.
Akizungumza wakati wa Jukwaa la DialogueNEXT lililoendeshwa na Wakfu wa Tuzo ya Chakula Duniani jijini Nairobi, Kagwe amesema kuwa tabia hiyo inakatisha tamaa ukuaji wa viwanda katika nchi zinazozalisha, inawafungia wakulima kuuza malighafi za bei nafuu na kubadilisha kazi za utengenezaji, mali na uwekezaji kwa uchumi wa kigeni.
Kagwe vile vile amedai kuwa kupanda kwa ushuru kumeizuia Afrika kuongeza ukuaji wa thamani wa kimataifa, na kulazimisha nchi zinazozalisha kahawa, chai, makadamia, pamba na ngozi kusambaza malighafi na kuagiza nje kama bidhaa zilizokamilika kwa bei ya juu.
Hata hivyo, amezitaka nchi za Afrika kupitisha sera zinazohimiza usindikaji wa ndani kabla ya kuuza nje, akisema marufuku ambayo imewekwa na taifa la Kenya ya mauzo ya nje ya makadamia ghafi inaonyesha mwelekeo ambao bara linafaa kuchukua.
Imetayarishwa na Maurine Amwayi
